Tanzania emblem

Ofisi ya Rais

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

Building photo

Sisi ni nani

Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ilianza kutekeleza shughuli zake kama Idara inayojitegemea kuanzia mwezi Julai, 2015 baada ya Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kupitisha muundo wa Idara tarehe 12 Februari, 2015.

Hata hivyo, Historia ya Idara ilianza mwaka 1963 wakati Baba wa Taifa, Mhe. Rais Julius Kambarage Nyerere alipotoa Waraka Na.7 wa mwaka 1963 ambao ulitoa mwongozo juu ya utunzaji bora wa nyaraka za Serikali. Waraka huo ulielekeza namna ya kutunza, kuhifadhi na kuteketeza nyaraka za Serikali. Mwaka 1965 Sheria ya Nyaraka za Taifa Na. 33 ilitungwa na Bunge ikiwa na maudhui ya kulinda na kuhifadhi urithi andishi wa Taifa letu. Sheria hii ndiyo ilianzisha rasmi Idara ya Nyaraka za Taifa.

Aidha, mwaka 1997 Serikali ya Awamu ya Tatu ilipitia upya miundo ya Wizara na Taasisi zake ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima Serikalini. Matokeo ya zoezi hili pamoja na mambo mengine yaliunda Divisheni mpya ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Divisheni hiyo mpya ilitokana na kuunganishwa kwa Idara ya Nyaraka iliyokuwa chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni na Sehemu (Section) ya Kumbukumbu iliyokuwa chini ya iliyokuwa Idara Kuu ya Utumishi kupitia tangazo la Serikali Na. 289 la tarehe 31 Oktoba, 1999.

Mnamo mwaka 2002 Bunge lilitunga Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Na. 3 ya mwaka 2002 ambayo ilifuta Sheria ya Nyaraka za Taifa Na. 33 ya mwaka 1965 na kuunda Idara mpya ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.

Vilevile mwaka 2004 Idara iliongezewa majukumu mengine baada ya Bunge kutunga Sheria Na. 18 ya mwaka 2004 ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa (Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume). Sheria hii inaipa Idara mamlaka ya kusimamia, kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na vitu vya Waasisi wa Taifa vyenye umuhimu wa kihistoria kwa Taifa letu.