Habari
SIMAMIENI SHERIA NA MIONGOZO ILI KUDHIBITI UPOTEVU WA NYARAKA-Mhe. Sangu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ametoa wito kwa Ofisi ya Rais-Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuweka utaratibu wa usimamizi wa Sheria na miongozo ili kuhakikisha Nyaraka za Taifa zinalindwa kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kubaini na kudhibiti mianya ya upotevu wa nyaraka katika taasisi za Umma ili kulinda usalama wa nchi.
Naibu Waziri Sangu, ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi ya Rais-Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na uadilifu ili kuepusha madhara makubwa kwa taifa yanayoweza kusababishwa na uzembe unaopelekea upotevu wa nyaraka.
Alisema kuwa utunzaji wa nyaraka ni jukumu adhimu linalohitaji viwango vikubwa vya usimamizi ili kuleta haki na uwazi katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali kwa kutumia nyaraka hizo.
Mhe. Sangu pia ameitaka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kutafuta mashirikiano na Taasisi nyingine ndani na nje ya nchi pamoja na kutoa elimu na ushauri wa kitaalam juu ya umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu kwa taasisi nyeti za Umma.
Aidha Mhe. Sangu ameipongeza Idara hiyo kwa namna wanavyofanya kazi kubwa ya kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanzania kwa kukusanya na kutunza kumbukumbu zao zitakazosaidia vizazi vijavyo kufahamu historia ya nchi kupitia waasisi hao.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vibali vya ajira na kuwezesha idadi ya watumishi kuongezeka kila mwaka kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bi. Editha Beda, wakati akitoa neno la shukrani amesema menejimenti imepokea maelekezo yote na kuahidi kuyafanyia kazi kwa ukamilifu ili kuongeza ufanisi katika utendajikazi kwa ustawi wa taifa.