Tanzania emblem

Ofisi ya Rais

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

Building photo

Habari

Taasisi za Umma zatakiwa kuweka mipango kuimarisha jitihada za serikali mtandao


 

Taasisi zote za umma nchini zimeelekezwa kuweka mipango itakayozisaidia kutatua changamoto ya urudufu wa mifumo ya TEHAMA ili kukuza na kuimarisha jitihada za serikali mtandao kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Maelekezo haya yametolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akifunga kikao kazi cha nne (4) cha serikali mtandao kilichofanyika jijini Arusha mapema wiki iliyopita na kushirikisha wadau zaidi ya 1300 wa serikali mtandao.
Mhe. Kikwete alisema kuwa utekelezaji wa mipango hii utasaidia katika kutimiza azma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na serikali ya kidijitali.
 “Ili kuweza kufikia mafanikio katika utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao, ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe ikiwa ni pamoja na taasisi kujiwekea mipango ya kutatua changamoto mbalimbali za TEHAMA zinazowakabili,” alisisitiza.
Aidha Mhe. Kikwete amewataka wataalam wa TEHAMA kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kutekeleza jitihada za serikali mtandao kupitia msaada na ushauri wa kitaalam unaotolewa na mamlaka hiyo kwa lengo la kuwasaidia watumishi kuijenga serikali ya kidijitali.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kutekeleza azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuijenga Tanzania ya kidijitali.
Alisema kuwa eGA imefanikiwa kuibadilisha nchi na utumishi wa umma kupitia sera na mbinu mbalimbali za utendaji kazi serikalini ili kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia TEHAMA.
Naibu Katibu Mkuu ameongeza kuwa kikao hiki kiwasaidie kujadili hali ya utekelezaji wa serikali mtandao katika taasisi za umma zikiwemo changamoto na mbinu za kukabiliana nazo ili kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba alisema kuwa miongozo, sera, sheria, kanuni pamoja na miradi ya ujenzi wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma nchini kutasaidia kupunguza urudufu wa mifumo, kurahisisha taasisi za umma kubadilishana taarifa na kuokoa fedha za umma kwa kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.
Kikao kazi hicho kilichoanza tarehe 06 Februari, 2024 na kuhitimishwa tarehe 08 kilibeba kaulimbiu isemayo “Uzingatiwaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Ubadilishanaji salama wa Taarifa”.